Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika. Hali hii inajidhihirisha kupitia matukio mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame na mafuriko. Athari za mabadiliko ya tabianchi zimeathiri sekta za kijamii na kiuchumi na maendeleo kama vile kilimo, utalii, nishati, maji, afya, mifugo na mifumo ikolojia ya bahari na hivyo kuathiri ongezeko la pato la taifa.
Ukame na mafuriko yamechangia gharama kubwa za kiuchumi, kuathiri maendeleo na maisha ya jamii za vijijini na mijini kwa pande zote za Tanzania Bara na Zanzibar. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inatakiwa kuweka utaratibu wa kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ili kulinda maendeleo yaliyofikiwa na kufikia maendeleo endelevu.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, jitihada hizo ni pamoja na; mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hufanyika katika sekta za nishati, usafirishaji, udhibiti wa taka, misitu, kilimo, shughuli za uzalishaji viwandani na matumizi ya bidhaa pamoja na matumizi mengine ya ardhi.
Inatarajiwa kuwa, miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta hizo itachangia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuchangia katika utunzaji endelevu ya mazingira na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi. Hivyo, Mwongozo huu unakusudia kuweka taratibu na matakwa kitaifa katika kusimamia na kudhibiti miradi ya biashara ya kaboni nchini.
2022 © Tatedo - Sustainable Energy Services Organization. All Rights Reserved. Designed by microsafi.com